![]() |
Mhariri mkuu wa Bongo5 Bw. Fredrick Bundara akiwa pamoja na mwariri msaidizi, Sandu George wakizungumza leo na waandishi wa habari katika uzinduzi wa Tuzo za watu 2015 |
Tuzo za watu zaja kivingine, vipengele vyaongezeka
Kampuni ya Bongo5 Media Group, imezindua msimu mpya na wa pili wa Tuzo
za Watu Tanzania zilizoanzishwa mwaka jana ili kuwatuza watu kwenye sekta
ya burudani na habari wanaofanya vizuri.
Akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari leo, mhariri mkuu
wa mtandao wa Bongo5, Fredrick Bundala amesema tuzo za mwaka huu
zimeboreshwa zaidi kwa kuongeza vipengele vitatu vipya.
“Mwaka huu tuzo zimeongezewa nguvu zaidi. Kutoka vipengele 11
tulivyokuwa navyo mwaka jana hadi vipengele 1. Mwaka huu tumeongeza
vipengele vitatu muhimu,” amesema Bundala.
Amevitaja vipengele vilivyoongezeka kuwa ni pamoja na muongozaji
wa filamu anayependwa, tovuti/blogu inayopendwa na mfadhili maarufu
anayependwa.
“Kwenye jamii yetu kuna watu maarufu ambao wamekuwa mstari wa mbele
kusaidia jamii hususan watu wasio na uwezo ama wanaoshi katika mazingira
magumu. Tumeona ni muhimu pia kuwatambua watu hawa ambao huamua
kujinyima na kugawana kile wanachokipata ili kuwasaidia watu wanaohitaji
msaada,” ameongeza.
Amesema zoezi la kuanza kupendekeza majina ya washiriki limeanza rasmi
Alhamis hii ambapo wananchi wanaweza kuwapendekeza kupitia website ya
www.tuzozetu.com ama kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu kwa kuandika neno
TZW, code ya kila kipengele na jina la anayependekezwa kwenda 15678.
“Baada ya wiki tatu kuanzia leo tutatangaza majina ya washiriki watano
waliochaguliwa kuingia kwenye awamu ya kwanza ya mchujo ambapo katika
kipindi cha wiki mbili itafanyika michujo mingine miwili ili kuwapata washiriki
watatu watakaoingia fainali,” amesisitiza Bundala.
“Washiriki watatu kwenye kila kipengele watahudhuria kilele cha tuzo hizo
kitakachofanyika katikati ya mwezi wa tano.”
Kwa upande wake mhariri msaidizi wa Bongo5, Sandu Mpanda, amesema
kuwa utofauti wa tuzo za watu na tuzo zingine ni kuwa wananchi wana nguvu
ya asilimia 100 kumchagua mshindi.
“Kura za wananchi ndizo zitakazompata mshindi. Ni muhimu wananchi
kuwapigia kura watu wanaowapenda ili kuhakikisha wanashinda vipengele
walivyotajwa kuwania,” amesema Mpanda.
Mpanda amevitaja vipengele vinavyowaniwa kwenye tuzo za mwaka huu
kuwa ni pamoja na Mtangazaji wa redio anayependwa (TZW1), Kipindi
cha redio kinachopendwa (TZW2), Mtangazaji wa kipindi cha runinga
anayependwa (TZW3), Kipindi cha runinga kinachopendwa (TZW4), Tovuti/
Blogu inayopendwa (TZW5) na Muongozaji wa video za Muziki anayependwa
(TZW6).
Vingine ni Muongozaji filamu anayependwa (TZW7), Mwigizaji wa
kike anayependwa (TZW8), Mwigizaji wa kiume anayependwa (TZW9),
Mwanamuziki wa kike anayependwa (TZW10), Mwanamuziki wa kiume
anayependwa (TZW11), Filamu inayopendwa (TZW12), Video ya Muziki
inayopendwa (TZW13) na Mfadhili maarufu (TZW14).
Hashtag za kwenye mitandao ya kijamii mwaka huu ni #TZW2015 na
#TuzozaWatu.
Twitter: @djmwanga
Instagram: @djmwanga
Facebook Fans Page: DJMwanga