Wimbo wa Ney wa Mitego umefungiwa rasmi,barua kutoka BASATA hii hapa..

Siku ya jana BASATA uongozi wa BASATA ulisema bado haujaufungia wimbo
wa Ney wa Mitego mpaka pale watakapofuata taratibu zote za kisheria.Leo
BASATA wametoa tamko rasmi kupitia barua waliyoituma kwenye vyombo vya
habari inayothibitisha kuwa wameufungia wimbo wa Shika adabu yako wa
msanii wa bongo fleva,Ney wa Mitego kutokana na wimbo huo kuwa na lugha
ya maudhi,udhalilishaji,uchochezi n.k na kutaka msanii huyo kutouongelea
wimbo huo popote kwenye vyombo vya habari.
Barua ya Basata hii hapa isome….
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 4 (1) (j) cha sheria ya BASATA
namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepwa mamlaka ya kuratibu na kufuatilia
mienendo ya mtu yeyote anayehusika na kazi za Sanaa na kuhakikisha
linalinda maadili ya kitaifa miongoni mwa Wasanii wanapokuwa jukwaani au
wanapobuni kazi yoyote ya Sanaa.
Aidha, kifungu cha 4 (2) cha sheria hii kinalipa Baraza nguvu ya
kisheria kufanya jambo lolote lile kuliwezesha kufanya majukumu yake kwa
faida na ustawi wataifa.
Baraza la Sanaa la Taifa limekuwa likipokea simu za maswali na
malalamiko kadhaa kutoka kwa waandishi wa habari na wadau wa Sanaa ambao
kwa njia moja ama nyingine wameguswa na kuchukizwa na kazi hiyo ambayo
si tu inadhalilisha tasnia ya Sanaa bali inawafanya watu makini kuanza
kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya Sanaa kwa ujumla.
BASATA mara kadhaa limekuwa likikemea na kuchukua hatua kadhaa dhidi ya
tabia hii chafu ambayo ilianza kujitokeza kwenye kampeni za uchaguzi
mkuu wa mwaka jana wa 2015. Kukemea huku ni kwa msingi mmoja kwamba
asili ya tasnia hii ya Sanaa ni kuelimisha jamii, kukosoa pale
kunapokuwa na tatizo, kuburudisha na kujenga jamii yenye staha, umoja wa
kitaifa, mshikamano na amani.
Ni wazi wasanii wengi wanafanya kazi zao vizuri, kwa kubuni kazi zenye
ubora, zenye kujenga jamii na zaidi zinazoburudisha rika zote kiasi cha
kuzifanya zililetee heshima taifa. Kati ya hawa wengi, kuna wachache
ambao wanaipaka matope tasnia ya Sanaa na kwa kiasi kikubwa wanaonesha
wazi kutokuwa na nia njema.
Kwa mantiki hii BASATA halitavumilia hawa ‘wasanii’ wachache ambao
wanataka kuigeuza tasnia ya Sanaa na wasanii genge la wahuni, wasio na
staha, wa kudharaulika na waliojipanga kuibomoa jamii na kuharibu amani
na utulivu uliopo nchini.
BASATA linapenda kueleza yafuatayo:
1. Vyombo vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya
Sanaa kabla ya kuingia kwenye mtego wa kuwa mawakala wa uharibifu wa
jamii kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa. BASATA lilishaziandikia radio
zote kuzishauri kuwa na kamati za maudhui ya kazi za Sanaa lakini
inashangaza baadhi ya vyombo vya habari vinakuwa vya kwanza kushabikia
nyimbo hizo chafu na kuwapa muda mrefu wa mahojiano wasanii hao na
baadaye kurudi BASATA kuhoji uhalali wa nyimbo husika. Hii si sawa hata
kidogo.
2. Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli
imejipanga kuwajengea mazingira bora ya utendaji Wasanii wote nchini
kupitia kuboresha miundombinu ya Sera, Sheria na Kanuni. Hata hivyo,
uwepo wa Wasanii kama hawa unafanya jamii kuhoji hadhi ya wasanii,
nafasi yao katika jamii na kwa maana hiyo kukatisha tamaa juhudi za
kuipa msukumo sekta hii maana wadau wakuu ambao ni wasanii wanaanza
kuoneasha kuwa mawakala wa uharibifu wa jamii.
3. BASATA linawataka wasanii kujiuliza mara mbili kabla ya kubuni kazi
zao za Sanaa. Wafikirie wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao
watazipokeaje? Wavae nafasi ya wale wanaowatukana na kuwadhalilisha,
Waelewe kwamba Sanaa si uwanja wa kutusi na kudhalilisha watu hata
kidogo. Ikitokea wale wanaotukanwa na kudhalilishwa kughafilika Sanaa
itakuwa uwanja wa vita. Hili halikubaliki.
4. Tunafahamu kuna wasanii wamekuwa wakifanya hivyo makusudi kutafuta
‘umaarufu uchwara’ ambao wanadhani utakuja kutokana na kuzungumziwa
sana. Tunapenda kusema wazi kwamba umaarufu hauji kwa upuuzi wa namna
hiyo unakuja kwa msanii mwenyewe kujiheshimu, kujituma, kubuni kazi bora
na zenye kulifahamu vema soko la ndani na la kimataifa.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
Source: Times Fm

Download DJMwanga Android Application Click HERE

https://goo.gl/Dpx8j4
JIUNGE NAMI KUPITIA 
Twitter: @djmwanga     
Instagram: @djmwanga     
Facebook Fans Page: DJMwanga
ad

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *